Friday, 3 March 2017

AJALI YA BASI YALETA MAJONZI SUA

Usiku wa Alhamisi ya tarehe 2 Feb 2017 uligeuka simanzi kwa Watanzania baada ya basi la abiri mali ya kampuni ya Ilyana kutokea Dar kwenda Songea kupata ajali maeneo ya Njombe .

Katika ajali hiyo watu watatu walipoteza maisha huku 28 wakijeruhiwa.Aidha, kati ya waliopoteza maisha, mmoja ni mwanamke na wawili ni wanaume.

Chanzo chetu cha habari kimeweza kupata jina la mmoja wa wanaume waliopoteza maisha kuwa ni Festo Nungu, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo kikuu cha Sokoine, katika Koleji ya Agriculture akiwa amebakisha semester moja kuhitimu shahada ya Kilimo mseto.

Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu wote pema peponi.
Bwana alitwaa Bwana ametwaa, jina la Bwana libarikiwe.Amina

Sunday, 12 February 2017

BARUA YA WAZI KWA RAIS

BARUAKWENDA KWA RAIS JPM ILIYOANDIKWA NA ANSBERT NGURUMO

Mheshimiwa Rais John Magufuli, sijawahi kukuandikia barua, ama ya sanduku la posta au ya mtandaoni. Leo nakuandikia kupitia gazetini kwa sababu mbili:-

Kwanza, natambua kuwa wewe ni msomaji wa magazeti. Naulishanithibitishia kuwa hukosi kusoma maandishi yangu. Kwa hiyo najua utasoma.

Bahati nzuri, ninachokuandika si siri. Ni barua ya wazi itakayosomwa na Watanzania wengine. Lengo la kuiweka wazi ni kukuhamasisha nawe utambue kuwa mawasiliano ya kujenga nchi hayahitaji kufanyikia sirini au gizani.

Hii itakufanya uelewe kwanini wananchi hawachoki kuhoji sababu za serikali yako kufuta matangazo ya bunge ya moja kwa moja. Nakwambia bila kificho kuwa, hata mjieleze vipi, wananchi hawako tayari kuelewa kuwa katika karne hii, bunge lao linaondolewa kwenye nuru na kuingizwa kwenye giza.

Mwanzoni, wananchi, wakiongozwa na wabunge, walimkasirikia Nape Nnauye, waziri uliyempa dhamana ya habari, sanaa, utamaduni na michezo, wakidhani ndiye aliamuru TBC, Shirika la Utangazaji la Taifa, lisitishe matangazo ya moja kwa moja kwa kisingizio cha gharama; kwa sababu ndiye aliyetoa tangazo hilo bungeni.

Lakini sasa wanaelewa kuwa Nape hawezi kufanya uamuzi mkubwa kama huo bila kutumwa na mkubwa wake wa kazi. Na kwa jinsi wanavyokufahamu wewe, kama Nape angekuwa amefanya uamuzi huo wa kijinga bila kukuhusisha au bila kutumwa na wewe, ungekuwa ama umetengua uamuzi huo au umemtumbua jipu.

Kwa sababu hiyo, wananchi wameachanana Nape, wanakuandama wewe, na sasa wanasema jipu hilo ni lako. Unaogopa kujitumbua kwa kuwa mganga hajigangi. Ndiyo maana nimeamua nikutumbue.

Pili, mimi na Watanzania wamegundua kuwa katika masuala mengi ya kitaifa, unadanganywa. Vijana wa mjini wanasema unaingizwa mkenge. Na ukishadanganywa, nawe unaibuka na kudanganya wananchi.

Naomba utambue kuwa kwa kusema haya siombi kazi kwako. Ninayo. Na sehemu ya majukumu yangu kwa taifa hili ni kuuambia wewe ukweli mchungu bila woga au upendeleo.

Tabia yangu hii inasaidia kuziba mapengo ya wasaidizi wako ambao, licha ya kwamba wapo katika majengo wanayoita ofisi, kimsingi hawapo kazini, kwa kuwa hawafanyi kazi yao, hasa ya kukushauri viizuri.

Na baadhi yao wanasema kwamba hushauriki, unafanya utakalo, mara nyingi, bila kupima madhara ya uamuzi wako.

Wanasema hii ndiyo sababu inayokufanya utoe kauli tata au zinazopingana mara kadhaa.

Kwa mfano, mtu mmoja ameandika kwenye mtandao wa kijamii, akinukuu kauli yako uliyotoa kwa hasira mwezi Februari 2016 baada ya MCC, Shirika la Changamoto za Milenia, la Marekani, kukata misaada kwa Tanzania kwa sababu ya wizi wa kura Zanzibar na kutunga sheria katili ya makosa ya mtandaoni.

Siku ile, ulisema hivi: “Haiwezekani nchi tajiri kama Tanzania tuwe ombaomba. Sisi ndio tunatakwa kuombwa misaada.”

Kauli yako ilizua gumzo nchi nzima. Baadhi ya wananchi, wakiwemo marais wastaafu, walisema kuwa misaada kutoka nje haikwepeki, na kwamba hata kama kauli yako ina ukweli wa kimantiki, si kweli katika uhalisia kwa kuwa serikali yako, haijajipanga kujitegemea na kujitosheleza.

Wengine walikudhihaki kuwa umetoa kauli hiyo mithili ya simulizi la sungura aliyeruka akashindwa kufikia mkungu wa ndizi, hatimaye akasema kwa hasira, “sizitaki mbichi hizi!!”

Vibaraka wako, wakiwamo wasaidizi wako, walitetea hoja yako. Mungu si Athuman, juzi umetoa kauli nyingine ulipotembelewa na Balozi wa Mareakani nchini, akaahidi kuipatia serikali yako msaada mkubwa wa dola milioni 800.

Katika furaha uliyokuwa nayo, ulisema hivi mbele ya waandishi wa habari:

“Amekuja balozi kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania, na anasema sasa hivi watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine tunaweza kusaini hata kesho wa dola milioni 410….Fedha za msaada kutoka Marekani ni muhimu mno kwa maendeleo ya Tanzania.”

Tuna marais wangapi? Februari ulisema hutaki misaada; Juni unasema misaada ni muhimu. Tunapouliza wasaidizi wako kwanini wanakuacha unatoa kauli za ajabu ajabu, wanasema hupendi kushauriwa.

Wanasema kuwa wanaogopa kukuambia usichotaka kusikia, kwa sababu wameshakusoma, unapenda kusikiliza sauti yako mwenyewe na kutanguliza hisia zako, badala ya kufanyia kazi ushauri wa wataalamu.

Eti wakati mwingine wanakuandikia hotuba za kirais katika matukio muhimu, ukishafika eneo la tukio unagoma kuzisoma; unatoa maoni yako ya kichwani, ambayo wakati mwingine yanakufanya uonekane kama kamanda wa polisi bada ya rais wa nchi.

Wanasema, kwa mfano, siku ya maadhimisho wa Wiki ya Sheria, maneno uliyotoa mbele ya wanasheria waliobobea, huku ukimwagiza jaji mkuu, yalikuwa yamekataa tenge, na hayatekelezeki kisheria; ni amri zisizofanana na mfumo wa kidemokrasia na utendaji wa kisheria.

Hawakukuambia pale pale, lakini walikuteta baadaye. Kwanini unaruhusu mambo haya yatokee wakati una nyenzo za kuyazuia?

Mmoja ameniambia wiki hii kuwa kwa jinsi anavyoona unazungumza na unatenda, una nia nzuri na taifa hili, lakini unakosa mbinu za kiuongozi. Anasema unatenda kama meneja, si kiongozi.

Anasema vitu vingine unavyoagiza, au unavyoamua, unavifanya kama mtawala, si kama kiongozi. Na kwa kukosa tunu ya uongozi, utafanya mambo mengi mazuri juu juu lakini hayatadumu kwa sababu hayakujengwa juu ya msingi imara.

Utakuwa umefanikiwa kufanya mambo mema kwa muda mfupi, lakini yatafutika kirahisi kwa kuwa mtindo uliotumika kuyatekeleza si endelevu, bali zima moto.

Wasaidizi wako wanakuficha mambo ya msingi. Wanasema umezidi ukali, na huna subira wala simile, kiasi kwamba unaweza kumwaibisha mtu yeyote mahali popote, bila kujali cheo au hadhi yake.

Na unawafanyia wenzako hivyo, lakini wewe hutaki kuguswa au kusahihishwa. Unalinda cheo chako, unadhalilisha vyeo vyao.

Kama ulikuwa hujajua, washauri wako sasa wana msimamo rasmi, kwamba watakushauri kwa kuzingatia kile unachotaka kusikia kutoka kwao.

Kama msimamo huu utadumu, mheshimiwa rais utaangamiza nchi. Kama unafurahia kuongoza nchi ya watu waoga, ujue nchi hiyo si Tanzania tunayotaka kujenga, au ile unayozungumzia kwenye hotuba zako.

Mazuri yote unayohubiri kwenye hotuba zako, yatatumika kukukejeli baada ya muda wako wa kukaa Ikulu kuisha.

Wanakutii, lakini hawakupendi. Na kwa sababu unawapuuza, wakipata fursa watakuhujumu.

Hata hivyo, wapo pia wanaodhani kwamba huna washauri wazuri. Mtu mmoja amesema; “Tatizo ninaloona sasa hivi, wasaidizi wa rais wanashindwa kutafsiri dira na ajenda yake. Hawamwelewi, naye haeleweki kwao.

“Apende asipende, anahitaji semina elekezi. Uamuzi unaochukuliwa na wasaidizi wake unatokana na tafsiri yao ya dira yake. Wengi wanafanya kwa woga na kulinda ajira zao tu.

“Panapohitajika ushauri wa kitaalamu wanapatwa na ugonjwa wa kupooza, kwa sababu wanaangalia matokeo ya kisiasa na uhusiano wao na rais. Tuanze kujiuliza, rais anaposema ‘Hapa Kazi Tu, ana maana gani?”

Huyu alisema hivi baada ya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya wanasiasa kwa sababu zile zile za miaka nenda rudi. Hawakui. Hawaelimiki. Na baadhi ya wakuu katika jeshi la polisi wanadai kuwa “wamefanya hivyo kwa kufuata “maagizo kutoka juu.” Huko juu ni wapi kama si Ikulu?

Uamuzi huu wa kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, kwa hofu kwamba itawafanya wananchi waelewe udhaifu wa serikali ya awamu ya tano, na kukuza upinzani ambao umesema mara kadhaa kwamba una nia ya kuuua, unakutia doa.

Uamuzi huu unakuondolea taswira ya ujasiri unayojijengea majukwaani unapokuwa unafoka. Sasa wananchi wanahoji: “Kumbe anafoka kuficha udhaifu wake!”

Ushauri, wangu kwako ni huu: Ongoza nchi, usiitawale. Acha wananchi wapumue. Zungumza nao, usiwahutubie. Sikiliza washauri wasiojikomba kwako.

Kumbuka kuwa nchi hii si ya rais na baraza la mawaziri, bali ni ya wananchi uliokuwa unawaomba kura na kuwaburudisha kwa maneno matamu na pushapu jukwaani. Hawa ndio waajiri wako. Wasikilize. Jifunze kwamba ubabe hautawali nchi yotote katika karne ya sasa.

Wananchi wanatazama mbele, hawatakubali kurudishwa nyuma, hata kwa mabavu

Friday, 10 February 2017

UTALII WA NDANI

Feb 10 2017 nilipata bahati ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya wanyama nchini Tanzania ijulikanayo kama Mikumi.

Mikumi ni hifadhi ya 4 kwa ukubwa ikitanguliwa na Serengeti, Ngorongoro na Manyara.

Hifadhi hii ipo katika mkoa wa Morogoro kati ya barabara iendayo Iringa.Ni hifadhi iliyosheheni wanyama wengi wa porini ikiwemo jamii ya swala,nyati,nyumbu, pundamilia, tembo, twiga, Simba na Chui.

Kilichonivutia zaidi ni juu ya Twiga.Huyu ni mnyama mwenye uwezo mkubwa wa kutofautisha rangi mbalimbali ikilinganishwa na wanyama wengine.Wao huweza tu kutofautisha nyeupe na nyeusi.

Mnyama huyo anapoona kitu kigeni hutulia mithili ya sanamu kwa ajili ya kuweza kukitambua na kama ni adui aweze kujua namna ya kujihami.

Kinachovutia zaidi ni mwondoko wake hasa anapotembea mwendo wa pole. Kutokana na muundo wa shingo yake pamoja na miguu yake, atembeapo mnyumbuliko Wa mwili wake huvutia mithili ya mwanadada mrembo awapo katika kupita mbele ya majaji ili apate kura za unenguaji.

Pamoja na hayo yote, Moyo Wa twiga huweza kukua hadi kufikia kilo 12 na hivyo hii humfanya kushindwa kuwa na mzunguko mzuri wa damu endapo atalala. Ili kuepusha shida, alalapo hukunja miguu na kulalia kifua, huku shingo ikiwa juu ama kuegeshwa kwenye mti.

Sunday, 29 January 2017

SAT212017

Ni Jumamosi ya tatu ya mwaka 2017 ambapo ilishihudiwa sherehe kubwa ya kumpongeza Shemasi Alfredi Fadhili Frimin huko kijijini kwao Kooti katika Kata ya Olele tarafa ya Mashati Wilayani Rombo Kilimanjaro.

Friday, 23 December 2016

Heri ya Krismasi na Mwakampya 2017

Anaandika *Nascent Franzwa*
Jmos Dec 24 2016

*Christmass ikufanye mtu bora*

Tarehe 25 kila Dec ni siku ambayo Wa Kristo walio wengi huitumia siku hiyo wakikumbuka ujio wa Masiha kwa mara ya kwanza duniani kupitia kwa Bikira aitwaye Marimu, zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Watu wengi huitumia siku hii kwa namna mbali mbali ikiwepo kufurahia na familia zao, kutembelea maeneo mbali mbali na kwa kusali.

Mara kadhaa katika sikukuu kubwa kama hii vimekuwepo visa kadhaa ambavyo vimekuwa vikisababisha maafa mathalani kuwaachia watoto kwenda katika kumbi za starehe za watoto ambazo hazina ubora na ulinzi wa kutosha.

Kama wazazi tunajukumu la kuhakikisha kuwa tutaacha vitabia hivyo na kuwa watu wapya kwa kuwa karibu zaidi na watoto wetu hasa wadogo ili kuepusha changamoto za maafa kwa watoto kujirudia.

Uongozi wa Marambamedia unawatakia watu wote sherehe njema za Kuzaliwa Kristo pamoja na Mwakampya wenye heri na fanaka.

Tuoneshe upendo kwa wote

©Marambamedia2016

Tuesday, 20 December 2016

MichezoniLeo2016Dec21

CAMEROON GIZA NENE
Jan 14 2018 kivumbi cha Afcon kitaanza kutimka kule Gambia. Hata hivyo, wakati mataifa shiriki yakiwa katika maandalizi, Cameroon huenda ikawakosa nyota wake saba kutokana na kile kocha wake Hugo Broos amekieleza kuwa ni maslahi binafsi ya nyota hao.

Nyota hao ni Beki mahiri wa Liverpool Joe Matip, Allan Nyom wa West Bromwich, Andre Onana wa Ajax Amsterdam, Guy N'dy Assembe wa Nancy, Maxime Poundje wa Girondins Bordeaux, Andre-Frank Zambo Anguisa wa Olimpique Marseille pamoja na Ibrahim Amadou wa Lille
(Chanzo: BBC)

REAL MADRID YAPATA AHUENI
Real Madrid imepunguziwa adhabu iliyotolewa na Fifa kutokana na kosa la kukiuka kanuni za usajili wa wachezaji wa umri wa chini ya miaka 18

Mahakama ya usuluhishi wa michezo(CAS) imewapunguzia adhabu hiyo kutoka kutosajili hadi Jan 2018 na badala yake kuanza usajili baada ya July 2017. Pia faini waliyotozwa na Fifa kwa kosa hilo imepunguzwa kutoka pauni 282,000 hadi Pauni 188,000.

VARY KUKOSA MECHI TATU
Mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy atalazimika kukaa nje ya Dimba hadi Jan 7 2018 ambapo atarejea wakati wa mchezo wao dhidi ya Everton kombe la FA mzunguko wa 3.
Hii ni baada ya rufaa ya timu yake kutupiliwa mbali na FA. Vardy alipewa kadi nyekundu alipomchezea vibaya Mame Diouf.
Michezo atakayoikosa Vardy ni ule wa Everton utakaochezewa ugenini katika dimba la Goodson Park, wa West Ham pale King Power na wa Middles brough Jan 02 018.

VPL MWISHO WA WIKI
Ijumaa hii 23Dec utakuwepo mtanange wa African Lyon vs Yanga watakaomenyana pale Shamba la Bibi saa kumi na nusu jioni.

Jumamosi 24Dec;
Majimaji vs Azam Fc uwanja wa Majimaji saa kumi kamili jioni.

Mwadui Fc vs Mbao Fc uwanja wa Mwadui Complex saa kumi kamili jioni.

Simba Sc vs JKT Ruvu Shamba la Bibi saa kumi kamili jioni.

©marambamedia.blogspot.com2016

Habari Kuu 20 Dec

Trump aidhinishwa rasmi kuwa Rais wa 45 wa Marekani.

Siku 32 za kupotea kwa Mwanaharakati wa Chama Kikuu cha upinzani nchini Tanzania , CHADEMA ,Ndg Ben Saanane bado ni fumbo zito.

Balozi wa Urusi nchini Uturuki Bwana Andrey Karlov auawa kwa kupigwa risasi akiwa katika ufunguzi wa maonesho ya sanaa. Rais Vladimir Putin amekitaja kitendo hicho kama uchokozi.

Mkurugenzi mtendaji wa mtandao maarufu Afrika Mashariki na Kati Jamii Forum Ndugu Maxence Melo aachiwa huru kwa dhamana huko nchini Tanzania.

Nchini DRC milio ya risasi imesikika maeneo kadhaa ya miji ikiwemo miji nikiwa ya Kinshasa na Lubumbashi kutokana na kutokuelewana kati ya upinzani na serikali juu ya muda wa nyongeza wa Joseph Kabila kusalia madarakani baada ya muhula wake kuisha usiku wa kuamkia Leo 20 Dec 2016.

Ripoti za shirika la Afya duniani zimeeleza kuwa, idadi inayokadiriwa kuwa sawa na nusu ya watu wazima barani Afrika wanakabiliwa na tatizo la Shinikizo la damu (Pressure) na hivyo kuifanya Afrika kuwa na kiwango cha juu cha tatizo hilo duniani kwa mujibu wa WHO.

Katika Michezo: Mwanadada Evelyene Njambi Thungu kutoka Kenya ameingia katika orodha ya warembo watano bora katika shindano la Malkia wa urembo duniani 2016 lililofanyika huko Marekani. Kwa sasa ndiye Malkia wa urembo barani Afrika.