Saturday, 11 November 2017

Mh Rais Magufuli azuru KSL

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Joseph Pombe Magufuli alikuwa Rais wa kwanza kuzuru kiwanda cha kuzalisha sukari, ambapo Kagera Sugar imepata bahati hiyo katika kipindi cha takribani miaka 14 pasipo viwanda vya sukari kupata bahati hiyo.
Siku ya Jumatano tarehe 8 November 2017, siku mbili baada ya uzinduzi wa jengo la kisasa la abiria la uwanja wa ndege wa Bukoba.
Rais Magufuli ambaye amejipambanua kwa Sera ya Viwanda, amekuwa akihubiri Maendeleo ya uchumi wa kati ambayo amejizatiti kuyafikia kupitia uimarishaji wa Sera ya Viwanda ili Tanzania iweze kuneemeka moja kwa moja na rasilimali nyingi ilizo nazo.
Aidha, pamoja na kukimwagia kiwanda cha Kagera Sugar sifa nyingi, pia aliwaomba wamiliki wa viwanda vya sukari nchini Tanzania kumhakikishia kutokuwepo kwa upungufu wa sukari nchini,ambapo pia aliwapa nafasi ya kuchukua tenda ya uagizaji wa Sukari msimu usiokuwa wa uzalishaji Sukari nchini.Kwa kuwapatia vibali hivyo, Rais ana imani kuwa  ataweza kuzuia mianya ya uagizaji holela wa Sukari nje ya nchi ambayo inapelekea baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuagiza Sukari isiyokuwa na ubora.

Aidha pia, Rais aliwaomba wazalishaji wote wa Sukari kuona ni namna gani wataweza kuongeza uzalishaji wa Sukari ili watakapofikia kiwango cha mahitaji kwa Taifa, aweze kuzuia kabisa uagizaji wa Sukari toka nje ya nchi.
Kiwango cha mahitaji ya sukari  kwa Mwaka ni takribani tani 450000 na upungufu takribani tani 130000.

Baada ya ziara hiyo Rais aliendelea na ziara yake ambapo alizuru taifa jirani la Uganda.